Shibuya kupanua marufuku ya unywaji pombe mitaani kwa mwaka mzima

Mamlaka za serikali za mitaa katika Kata ya Shibuya jijini Tokyo zinapanga kupiga marufuku unywaji pombe mitaani karibu na Kituo cha treni cha Shibuya kwa mwaka mzima.

Hatua hiyo inatokana na ombi kutoka kwa maduka katika eneo hilo, na huenda itaanza saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na moja asubuhi.

Kwa sasa sheria inazuia unywaji pombe wa usiku mitaani na katika bustani katika vipindi na matukio fulani, kama vile Halloween na likizo za mwisho wa mwaka.

Maafisa wanapanga kuwasilisha rasimu ya marekebisho ya sheria hiyo katika mkutano wa Kata ya Shibuya mwezi huu na kuona mabadiliko hayo yakitekelezwa mwezi Oktoba.

Sheria hiyo ilianza kutekelezwa mwanzoni mwaka wa 2019 ili kushughulikia msururu wa matatizo yanayohusu pombe wakati wa Halloween.

Kunywa pombe mitaani kumekuwa jambo la kawaida miongoni mwa vijana na watalii wa kigeni tangu mamlaka zilipolegeza hatua za kukabiliana na virusi vya korona.

Meya wa Shibuya Hasebe Ken anasema marufuku hiyo mpya inatokana na nia ya kata hiyo. Pia anasema anatumai watu wanafurahia kunywa kwenye baa na migahawa.