Majadiliano ya Shangri-la: Maafisa wa ulinzi kujadili Taiwan na Bahari ya China Kusini

Maafisa wa ulinzi kutoka Asia na nchi za Magharibi wameanza mkutano wa siku tatu nchini Singapore jana Ijumaa uitwao Majadiliano ya Shangri-la. Wanatarajiwa kujadili masuala ya usalama ya Asia, ikiwemo Taiwan, Bahari ya China Kusini na Korea Kaskazini.

Washiriki ni pamoja na Mawaziri wa Ulinzi Lloyd Austin wa Marekani, Kihara Minoru wa Japani na Dong Jun wa China. Vyanzo vya kidiplomasia vinasema Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy pia atashiriki.

Mapema jana Ijumaa, Austin na Dong walifanya mkutano tofauti. Ulikuwa ni mkutano wa kwanza wa ana kwa ana baina ya wakuu hao wa ulinzi katika nchi zao katika kipindi cha karibu mwaka mmoja na nusu.

Maafisa wa Marekani na China wanasema Austin na Dong walikubaliana kuendeleza majadiliano kati ya maafisa wa ulinzi. Lakini pande hizo mbili zilishindwa kupunguza tofauti zao kuhusu Taiwan na Bahari ya China Kusini.

Kikao cha kujadili ushirikiano miongoni mwa walinzi wa pwani kutoka nchi washiriki kitafanyika kwenye mkutano huo kwa mara ya kwanza.

Mawaziri wa ulinzi wa Japani na China wamepangiwa kufanya mkutano katika siku ya pili ya mkutano huo.