Maswali na Majibu: Ajali za kawaida za bidhaa katika msimu wa mvua na joto (5)

(5) Ajali za moto zinazosababishwa na feni za umeme zinazobebeka

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Matumizi mabaya ya bidhaa za umeme yanaweza kusababisha matatizo yasiyotarajiwa, na baadhi ya ajali hutokea mara kwa mara katika msimu fulani zaidi ya nyakati zingine za mwaka. Mfululizo huu unaangazia ajali za bidhaa ambazo hutokea mara kwa mara katika msimu wa mvua na joto. Kipengee cha hii leo kinahusu hatari za feni za umeme zinazobebeka unazoweza kuzibeba na kuzitumia.

Idadi inayoongezeka ya watu wanatumia feni za umeme zinazobebeka katika miaka ya hivi karibuni kwa sababu ya joto kali katika msimu wa joto. Betri za ayoni ya Lithiyamu zinatumika katika nyingi ya feni kama hizo.

Taasisi ya Taifa ya Teknolojia na Tathmini (NITE) inaonya kwamba iwapo watu wataziangusha feni hizo, betri hizo zinaweza kutoa moshi ama kushika moto kutokana na athari za kuanguka ardhini.

NITE inatoa wito kwa watumiaji kuzitumia feni zao kwa uangalifu. Inawaomba kuacha kutumia bidhaa hizo na kuwasiliana na watengenezaji ama mawakala wake wa mauzo ikiwa betri hizo zitapata mtikisiko.

Taasisi hiyo pia inatoa wito kwa watu kununua bidhaa madhubuti kwa sababu baadhi ya feni zinazobebeka zinauzwa mtandaoni bila ya taarifa za mtengenezaji, na baadhi ya maduka huwa hayatoi majibu tatizo linapotokea.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 31, 2024.