Kasri la Matsumoto linaongoza kati ya makasri ya Kijapani kwa wafuasi wa mtandao wa Instagram

Kasri la Matsumoto lililoko katika Mkoa wa Nagano katikati mwa nchini Japani limepita makasri mengine makubwa nchini humo kwa kuwa na wafuasi wengi zaidi wa mtandao wa Instagram.

Maafisa wa Jiji la Matsumoto wanasema idadi ya wafuasi wa akaunti ya Instagram ya kasri hiyo ilipita ile ya Kasri la Kumamoto lililopo kusini magharibi mwa Japani siku ya Jumanne wiki hii.

Kufikia Ijumaa mchana, Kasri la Matsumoto lilikuwa na wafuasi 28,906, 584 zaidi ya mshindani wake wa karibu.

Likiwa limejengwa zaidi ya miaka 400 iliyopita, Kasri la Matsumoto linajulikana kwa rangi yake nyeusi ya nje, na limeteuliwa kama urithi wa kitaifa.

Maafisa watatu wa jiji hilo ndio wanaosimamia akaunti hiyo ya Instagram, iliyofunguliwa mwaka 2021. Wanachapisha picha za kasri hilo katika misimu minne na matukio mbalimbali.

Kati ya machapisho yake takribani 600, picha inayoonyesha kasri hilo lilivyofunikwa na theluji imepata "alama za kupendwa" zaidi ya 78,000.

Mji wa Matsumoto umekuwa ukifanya kazi ili kuvutia watalii wa ndani. Rekodi ya watalii wa kigeni wapatao 160,000 walitembelea kasri hilo mwaka wa fedha uliopita ambao uliendelea hadi Machi mwaka huu.

Akaunti ya Instagram ya Kasri la Matsumoto ina maoni kwa lugha za Kiingereza, Kichina, Thai na lugha zingine. Wageni ni takribani asilimia 20 ya wafuasi wake.