Trump apatikana na hatia, hukumu kutolewa Julai 11

Donald Trump amekuwa rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kuwahi kupatikana na hatia. Baraza la mahakama jijini New York limemkuta na hatia ya makosa yote 34 yanayohusiana na malipo ya kumnyamazisha nyota wa filamu za watu wazima kabla ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2016.

Waendesha mashtaka wanasema Trump aliongoza njama ya kushawishi matokeo ya uchaguzi huo. Wanasema alificha malipo ya dola 130,000 yaliyofanywa ili kumnyamazisha muigizaji Stormy Daniels juu ya kukutana naye kingono.

Baada ya majuma kadhaa ya kusikilizwa kesi hiyo na siku mbili za mashauriano, baraza la mahakama lenya watu 12 lilikubaliana na hoja zao.

Trump anashikilia kwamba hana hatia, na anadai uamuzi wa mahakama umechochewa kisiasa. Alisema, “Nchi yetu yote inaibiwa hivi sasa. Hili limefanywa na utawala wa Biden ili kumjeruhi ama kumuumiza mpinzani wake, mpinzani wa kisiasa.”

Trump anaweza kukabiliwa na kifungo cha nje au hadi miaka minne gerezani. Hukumu dhidi yake imepangwa kutolewa Julai 11—siku chache tu kabla ya Mkutano wa kitaifa wa chama cha Republican kuanza huko Wisconsin, anakotarajiwa kushinda uteuzi.

Chini ya katiba ya Marekani, kupatikana na hatia kwa Trump hakumzuii kushiriki uchaguzi wa urais. Pia anatarajiwa kukata rufaa kupinga uamuzi huo, mchakato unaoweza kuchukua miezi kadhaa.

Rais Joe Biden wa Marekani alizungumzia uamuzi huo katika mitandao ya kijamii kwa kutuma ujumbe uliosema, “Kuna njia moja tu ya kumwondoa Donald Trump kutoka Ikulu ya Marekani: Kwenye sanduku la kupigia kura.”