Waziri wa Ulinzi wa Israel asisitiza umuhimu wa operesheni za kijeshi mjini Rafah

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema nchi hiyo ina taarifa za kina kuhusu mateka wanaoshikiliwa mjini Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza. Amesisitiza umuhimu wa kufanya operesheni za kijeshi mjini humo.

Wizara ya Ulinzi ya Israel ilisema jana Alhamisi kuwa Gallant alitoa maoni hayo alipozungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin.

Jeshi la Israel lilitangaza juzi Jumatano kuwa vikosi vyake vimechukua udhibiti wa Ushoroba wa Philadelphi, ambao ni ardhi yenye urefu wa takribani kilomita 14 kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri.

Israel inadai kwamba silaha na bidhaa zingine zinaingizwa kimagendo kutoka Misri hadi Gaza kupitia eneo hilo. Imesema vikosi vyake viligundua takribani mahandaki 20 kwenye eneo hilo na vinayachunguza na kuyaharibu.

Wakati huo huo, mamlaka za afya huko Gaza zilisema jana Alhamisi kuwa zimethibitisha vifo vya watu 53 kwenye eneo hilo katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Zimesema idadi ya vifo katika eneo la Gaza tangu Israel ilipoanza mashambulizi yake Oktoba 7 mwaka jana imeongezeka hadi 36,224.

Mpango wa Chakula Duniani, WFP ulisema jana Alhamisi kuwa viwango vya njaa katika maeneo ya katikati na kusini mwa Gaza vinaongezeka kwa kasi na kutoa wito kwa mamlaka za Israel kuruhusu upelekwaji wa misaada ya kibinadamu.