Korea Kaskazini yasema ilifanya ‘maonyesho ya kurusha roketi kubwa zaidi’

Korea Kaskazini inasema imefanya maonyesho ya urushaji yanayohusisha vifaa vikubwa zaidi vya kurushia roketi kadhaa. Tangazo hilo linakuja siku moja baada ya nchi hiyo kuripotiwa kurusha makombora ya balistiki.

Gazeti la chama tawala cha Wafanyakazi la Rodong Sinmun nchini Korea Kaskazini liliripoti hili leo Ijumaa. Linasema kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un alisimamia urushaji wa roketi hiyo ya milimita 600.

Picha inaonyesha makombora 18 yakirushwa wakati mmoja kutoka kwenye vifaa vya kurushia vinavyosogea.

Ripoti hiyo inasema warushaji makombora hayo walipiga kisiwa kilicholengwa kilichopo umbali wa kilomita 365. Vyombo vya habari vya Korea Kusini vinasema kambi kuu ya anga iliyopo nchini humo itakuwa ndani ya umbali wa kombora hilo.

Korea Kaskazini inadai kuwa makombora hayo yana uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia. Inaongeza kuwa maonyesho hayo yalifanywa ili kuonyesha kuwa nchi hiyo haitasita kutangulia kufanya mashambulizi dhidi ya Korea Kusini.