Maswali na Majibu: Ajali za bidhaa za kawaida katika msimu wa mvua na joto (4)

(4) Ajali iliyotokana na joto kali

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Matumizi mabaya ya bidhaa za umeme huweza kusababisha matatizo yasiyotarajiwa, na baadhi ya ajali hutokea mara kwa mara katika msimu fulani zaidi ya nyakati zingine za mwaka. Mfululizo huu unaangazia ajali za bidhaa ambazo hutokea mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua na joto. Kipengele cha hii leo, ni kuhusu hatari za kuacha bidhaa fulani kwenye gari wakati wa msimu wa joto.

Taasisi ya Taifa ya Teknolojia na Tathmini (NITE) inasema kwamba mnamo Oktoba mwaka 2022, kiti cha gari kiliwaka moto baada ya betri ya simu ya mkononi iliyoachwa kwenye gari lililokuwa limeegeshwa nje mkoani Hyogo kushika moto. Taasisi hiyo inasema joto la nje lilikuwa karibu nyuzijoto 30 za selisiasi na moto ulianza karibu saa mbili baada ya gari hilo kuegeshwa. Inaamini kuwa betri iliyokuwa imeachwa kwenye joto kali garini ilikuwa chanzo cha moto huo. Betri nyingi za simu za mkononi ni za ayoni ya lithiyamu. Betri hizo nyepesi na zenye ubora wa juu zinatumika sana kwenye bidhaa za kielektroniki kama vile simu za smartphone na kompyuta binafsi. Lakini athari za mgongano ama joto linaweza kusababisha betri kulipuka ama kushika moto. Ni hatari sana kuziacha bidhaa hizi ndani ya gari linaloweza kukumbwa na joto kali. Bidhaa zinazotumia gesi kama vile dawa za kuzuia wadudu na vinyunyizo vya kupooza, pia zinaweza kulipuka kwenye joto kali, hivyo tafadhali kuwa makini na mahala unapoziweka.

Taarifa hii ni sahihi kuanzia Mei 30 mwaka 2024.