UN yaonya juu ya maporomoko zaidi ya ardhi Papua New Guinea

Imekuwa karibu wiki moja tangu maporomoko ya ardhi yaliyosababisha vifo kuikumba Papua New Guinea. Afisa wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, UNDP alisema kuna dharura ya kuwahamishia wakazi maeneo salama, kwani eneo kulikotokea maporomoko hayo Ijumaa iliyopita bado si thabiti.

Mate Bagossy ni Mshauri wa Masuala ya Binadamu wa UNDP nchini Papua New Guinea. Alizungumza na NHK jana Alhamisi kuhusiana na ziara yake ya hivi karibuni katika kijiji kilichokumbwa na janga hilo katika jimbo la milimani la Enga.

Alisema, “Barabara ambayo baadhi ya sehemu zimefunikwa na maporomoko ya ardhi inazama. Kuna miti ambayo inainama, ikiwa ni pamoja na katika maeneo yasiyokuwa karibu kabisa na eneo palipotokea maporomoko yenyewe ya ardhi, ikimaanisha kuna harakati fulani zinazoendelea ardhini.”

Shehena ya kwanza ya msaada wa Australia yenye chakula na dawa, iliwasilishwa katika eneo hilo la mbali jana Jumatano.

Bagossy alisema bidhaa muhimu zinazopelekwa kijijini humo kwa sasa hazitoshi. Lakini aliongeza kuwa msaada zaidi unaonekana upo njiani.

Akirejelea makadirio ya serikali kwamba zaidi ya wanakijiji 2,000 wamefunikwa chini ya vifusi na matope, Bagossy alisema idadi halisi haijabainika. Aliongeza kuwa, “Ninaamini kwamba baadhi ya takwimu zilizojumuishwa huenda ni makadirio yaliyopita kiasi. Lakini ni dhahiri hili ni janga kubwa.”

Watu sita wamethibitishwa kufariki katika janga hilo. Shirika la umma la utangazaji la Australia liliripoti kwamba zaidi ya watu 160 walifukiwa wakiwa hai, likiwanukuu maafisa wa eneo hilo.