KDDI yaahidi kujenga mfumo wa mawasiliano mwezini

Kampuni kubwa ya mawasiliano ya KDDI ya Japani inasema inapanga kujenga mfumo wa mawasiliano Mwezini. KDDI inatumai kuanza huduma hizo mwaka 2030 wakati utafiti wa mwezi ukishika kasi kote duniani.

Kampuni hiyo ilisema jana Alhamisi kuwa itajenga muundombinu wa mwezi ili kuwezesha mawasiliano ya data yenye kasi ya juu kati ya wanaanga na vyombo vya utafiti mwezini.

Kufikia mwaka 2028, KDDI inalenga kuanzisha mitandao ya mawimbi ya redio na mwanga ya kiwango cha juu inayounganisha Mwezi na Dunia.

Mpango huo unajumuisha pia kuendeleza teknolojia itakayowezesha mwangaza wa leza kusafiri umbali wa kilomita 380,000 kati ya Dunia na Mwezi.

Kampuni hiyo inataka kuongeza kasi katika uendelezaji wa roboti zitakazotumika kujenga kituo cha mawasiliano.

KDDI pia itashirikiana na makampuni mengine yanayoibukia kuanzisha biashara mpya katika anga za juu.

Mpango unaoongozwa na Marekani wa Artemis unalenga kutuma wanaanga mwezini mwaka 2026 au baadaye. Mwezi uliopita, Marekani na Japani zilikubaliana kuwa wanaanga wa Japani watakuwa miongoni mwa wale watakaotumwa Mwezini.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya KDDI Matsuda Hiromichi anasema, “Popote aendapo binadamu, nyakati zote kuna hitaji la mawasiliano bora. Tunadhamiria kutoa msaada madhubuti kwa juhudi hizi.”

Matsuda anasema anafahamu kuwa uwekezaji wa awali ni muhimu ili kuboresha biashara ya anga za juu katika siku zijazo.