Xi aahidi msaada zaidi kwa Gaza, atafuta uhusiano thabiti na mataifa ya Kiarabu

Rais wa China Xi Jinping ameahidi msaada zaidi wa yuan milioni 500 au takribani dola milioni 69 kwa Ukanda wa Gaza katika mkutano wa ngazi ya mawaziri na mataifa ya Kiarabu.

Msaada huo unaonekana kama hatua ya kuongeza ushawishi wa China Mashariki ya Kati huku Marekani ikichukua msimamo wa kuiunga mkono Israel.

Xi alizungumza jana Alhamisi kwenye mkutano wa maafisa waandamizi wa Kongamano la Ushirikiano wa China na Mataifa ya Kiarabu uliofanyika mjini Beijing nchini China.

Xi aliuambia mkutano huo kwamba China itafanya kazi na mataifa ya Kiarabu kuufanya uhusiano wao kuwa wa mfano katika kudumisha amani na uthabiti wa dunia. Aliashiria kuwa China inataka kuimarisha ushirikiano katika nyanja kama vile teknolojia ya Artificial Intelligence, AI, nishati na biashara.

Kuhusiana na mgogoro kati ya Israel na Palestina, Xi alisema, “vita havipaswi kuendelea daima” na “dhamira ya suluhisho la mataifa mawili haipaswi kuyumbishwa kwa makusudi.”

Alithibitisha tena usaidizi wa China katika kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina. Aidha Xi aliahidi msaada zaidi katika kusaidia kupunguza janga la kibinadamu huko Gaza pamoja na kusaidia ujenzi upya baada ya vita.