Mafuriko makubwa yanaendelea kuathiri watu kusini mwa Brazil

Watu kusini mwa Brazil wanaendelea kuathiriwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa tangu mwishoni mwa mwezi Aprili.

Mamlaka katika jimbo la Rio Grande do Sul zinasema watu 169 wamethibitishwa kufariki na watu 44 hawajulikani waliko kufikia jana Jumatano.

Maeneo mengi ya mji mkuu wa jimbo la Porto Alegre yamefunikwa na maji kwa zaidi ya siku 20. Wakazi wengi wamelazimika kuhama kwa muda mrefu.

Watu wengi wenye asili ya Kijapani wanaishi katika eneo hilo. Ofisi ya shirika linalotoa huduma za matibabu majumbani kwa watu hao ilifunikwa kwa mita 3 za maji ya mafuriko kwa wakati fulani. Mita moja ya maji bado imefunika ofisi katika sehemu ya kaskazini mwa jiji.

Maeneo yaliyokumbwa na maafa yanatafuta msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa huku wasiwasi mkubwa ukiongezeka juu ya usalama na kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza.