Israel inatarajia kundeleza mapigano Gaza hadi mwisho wa mwaka

Afisa mmoja mwandamizi wa Israel ameashiria kuwa operesheni za kijeshi za nchi yake katika Ukanda wa Gaza huenda zitaendelea mwaka huu wote.

Afisa huyo ambaye ni Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Israel Tzachi Hanegbi alizungumza na chombo cha habari cha nchini humo jana Jumatano.

Alisema nchi yake inatarajia miezi saba mingine ya mapigano ili kuharibu uwezo wa kiserikali na kijeshi wa kundi la Kiislamu la Hamas.

Jeshi la Israel jana Jumatano liliendelea na mashambulizi katika eneo hilo.

Vyombo vya habari vya eneo hilo vilisema mashambulizi ya anga katika nyumba moja huko Rafah, kusini mwa Gaza, yamesababisha vifo vya watu wanne, wakiwemo watoto watatu. Watu 15 wameripotiwa kuuawa ndani ya saa 24 zilizopita.

Mamlaka ya afya ya Gaza imesema idadi ya vifo katika eneo hilo imeongezeka hadi 36,171 tangu kuanza kwa mgogoro wa Israel na Hamas Oktoba mwaka jana.