Maswali na Majibu: Ajali za bidhaa za kawaida katika msimu wa mvua na joto (3)

(3) Ajali zinazosababishwa na vifaa vya kielektroniki vikiwekwa kwenye maji

NHK inajibu maswali yanahohusiana na kuhakikisha usalama wa maisha ya kila siku. Matumizi mabaya ya vifaa vya umeme huenda yakapelekea matatizo yasiyotarajiwa, na baadhi ya ajali hutokea mara nyingi katika msimu fulani kuliko nyakati zingine za mwaka. Katika makala hii tunaangazia ajali za bidhaa ambazo mara nyingi hutokea wakati wa msimu wa mvua na ule wa joto. Katika sehemu ya tatu, tutazungumzia kuhusu ajali zinazosababishwa na vifaa vya kielektroniki ambavyo vimekuwa vikiwekwa kwenye maji.

Taasisi ya Taifa ya Teknolojia na Tathmini (NITE) inaripoti ajali nyingi zinazohusiana na vifaa vya kielektroniki kushika moto baada ya kuloa maji. Mwezi Julai mwaka 2015, mtumiaji mmoja katika mkoa wa Osaka alikuwa akijaza nishati kwenye kamera yake ya kidigitali ambayo ilikuwa ikitumika baharini. Baada ya kugundua kuwa kamera yake ilikuwa ikipata joto lisilo la kawaida, mtumiaji huyo alichomoa waya wa kuongezea nishati wakati moto ulipoanza kuwaka katika sehemu ya maungio. NITE inaamini maji yaliyobaki ndani ya maungio yalisababisha shoti, na kupelekea kutokea joto lisilo la kawaida. Taasisi hiyo inatoa wito kwa watumiaji kuchukua hatua stahiki za kudumisha ukavu na kuvikausha vifaa visivyopenyesha maji kabla ya kuviweka nishati tena, huku angalizo likiwa katika maungio ya waya wa kuwekea nishati. Katika vifaa vinavyoruhusu maji kuingia, watumiaji wanashauriwa kufuata maelekezo ama kumuuliza mtengenezaji ikiwa ni salama kuendelea kuvitumia.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 29, 2024.