Wabunge nchini Georgia wapitisha muswada wa 'ushawishi wa kigeni'

Wabunge nchini Georgia wanasonga mbele na sheria ambayo imezua maandamano makubwa. Walipiga kura jana Jumanne kupinga kura ya turufu ya rais kuhusu sheria hiyo, ambayo inayataka mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari vinavyopokea asilimia 20 ya ufadhili wao kutoka ng'ambo kujiandikisha kama "mawakala wenye ushawishi wa kigeni."

Chama tawala kinasema sheria hiyo ni "muhimu kabisa" kwa mustakabali wa Georgia. Hata hivyo, wabunge wa upinzani wanahofia kuwa itatumika kupunguza shughuli za watu ambao serikali inaona kuwa hawafai.

Rais Salome Zourabichvili alitoa wito kwa watu kupiga kura za maoni kuipinga sheria hiyo. Aliwauliza watu wa Georgia kwenye mitandao ya kijamii kama wanataka "uelekeo wa kiulaya" au "utumwa wa Urusi."

Maandamano makubwa yameendelea kwa majuma kadhaa. Waandamanaji wanasema demokrasia yao iko hatarini na kwamba chama tawala kinajaribu kuitenga Georgia kutoka mataifa ya Magharibi na kuifanya "mshirika wa Urusi."

Georgia inatuma ombi la kujiunga na Umoja wa Ulaya. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema "anasikitishwa" na uamuzi wa wabunge.