Waandamanaji kote duniani walaani shambulio la anga mjini Rafah

Vikosi vya Israel vimekaidi agizo lililotolewa siku ya Ijumaa wiki iliyopita na Mahakama ya Kimataifa ya Haki la kusitisha mashambulizi yao mjini Rafah, kusini mwa Gaza. Vikosi hivyo vilianzisha shambulizi la anga mwishoni mwa wiki ambalo mamlaka za afya katika eneo la Gaza zinasema kuwa watu wasiopungua 45 waliuawa. Shambulio hilo limezua ukosoaji kote duniani.

Juzi Jumatatu waandamanaji nchini Hispania walisema hawataki kuwa "washiriki" wa kile wanachokiita "mauaji ya halaiki." Viongozi wao wa kisiasa walijiunga na wale wa Ireland na Norway wiki iliyopita ili kuongeza mataifa yao kwenye idadi ya zaidi ya mataifa mengine 140 ambayo yameutambua utaifa wa Palestina. Waandamanaji jijini Istanbul nchini Uturuki pia walipaza sauti zao walipokuwa wakielekea kwenye ubalozi mdogo wa Israel.

Vikosi vya Israel havijasitisha mashambulizi yao huko Rafah. Shirika la habari la Reuters lilitoa taarifa ya mashahidi wakisema kuwa vifaru vimeingia katikati mwa jiji kwa mara ya kwanza.