Msaada wa kigeni waelekea Papua New Guinea kufuatia maporomoko ya ardhi

Papua New Guinea imetoa wito wa msaada kwa nchi jirani ili kukabiliana na maporomoko ya ardhi ya Ijumaa iliyopita yaliyosababisha vifo.

Timu ya usaidizi wa kukabiliana na janga ya Australia imepelekwa kwenye nchi hiyo kusaidia juhudi za uokoaji na ujenzi mpya. Serikali ya Australia imesema inatoa zaidi ya dola milioni moja na nusu za msaada wa kibinadamu.

Waziri Mkuu wa Australia, Antony Albanese juzi Jumanne alisema nchi yake inatoa vitu vya msaada wa dharura, ikiwemo makazi, vifaa vya usafi na msaada maalum kwa wanawake na watoto.

Nchi zingine, ikiwemo New Zealand na India, pia zinatoa misaada. New Zealand imesema inapeleka ndege za kijeshi ili kusambaza misaada.

Sehemu ya mlima kwenye jimbo la kaskazini la Enga ilianguka Ijumaa iliyopita. Watu sita wamethibitika kufariki, lakini inahofiwa idadi ya vifo huenda hatimaye ikafikia mamia kadhaa ama zaidi.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba jumla ya watu karibu 8,000 wameathirika, wakiwemo wale wanaohitaji kuhamishwa.

Oparesheni za uokoaji na ujenzi mpya zimekwamishwa na hatari ya kutokea maporomoko zaidi na kwa sababu barabara kuu na zingine, hazipitiki.