Kikundi kazi cha Umoja wa Mataifa kinaitaka Japan kuunda taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu

Kikundi kazi cha Baraza la Haki za Kibinadamu cha Umoja wa Mataifa, UN kinatoa wito kwa Japani kuanzisha taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu, ikiwa ni miongoni mwa mapendekezo mbalimbali.

Kikundi Kazi cha Biashara na Haki za Kibinadamu kimetoa ripoti kulingana na uchunguzi wake wa kwanza uliofanywa nchini Japani kati ya Julai na Agosti mwaka jana.

Ripoti hiyo inasema kikundi hicho kina wasiwasi mkubwa kuhusu "ukosefu wa taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Japani," na kutokuwepo kwake "kunaweza kutatiza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki na utatuzi madhubuti." Inataka kuanzishwa kwa taasisi kama hiyo.

Ripoti hiyo pia inarejelea suala la pengo la kijinsia katika mishahara na uwakilishi mdogo wa wanawake katika nyadhifa za utendaji, pamoja na mishahara na afya ya wafanyakazi wanaohusika kusafisha na kufunga kabisa mtambo wa nyuklia wa Fukushima namba moja ulioharibika. Pia ilibainisha saa nyingi za kazi katika tasnia za anime.

Maoni ya serikali ya Japani pia yamewekwa hadharani pamoja na ripoti hiyo. Japani inasema inaamini kuwa baadhi ya taarifa katika ripoti hiyo "zina mambo ambayo yanaonekana kuwa si sahihi au madai ya upande mmoja."

Ripoti hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la UN mwishoni mwa mwezi Juni.