Ushindi wa chama tawala hatarini katika uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini

Watu nchini Afrika Kusini wamepiga kura zao katika uchaguzi mkuu huku wingi wa viti wa chama tawala bungeni ukiwa hatarini.

Upigaji kura ulifanyika jana Jumatano. Afrika Kusini hufanya uchaguzi mkuu mara moja kila baada ya miaka mitano. Katika jiji la Johannesburg, watu wengi walipanga foleni mbele ya vituo vya kupigia kura.

African National Congress, ama ANC, imekuwa madarakani kwa miaka 30.

Lakini wafuatiliaji wanasema rushwa imeenea kwenye taasisi za serikali chini ya utawala wa muda mrefu wa ANC. Wanasema ukarabati na usimamizi wa miundombinu ya msingi haufanyiki inavyotakiwa, hivyo kusababisha kukatika kwa maji na umeme mara kwa mara.

Uchumi wa Afrika Kusini umekumbwa na mkwamo, huku kukiwepo na ukosefu mkubwa wa ajira na kupanda kwa bei.

Nchi hiyo inakabiliwa na kuzorota kwa usalama kwani vitendo vya mauaji na uhalifu wa kutisha vimekithiri.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vinaripoti maoni kwamba wingi wa viti vya ANC katika uchaguzi huo huenda ukashuka hadi chini ya asilimia 50 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 na kwamba chama hicho kinaweza kupoteza wingi wa viti bungeni.

Uchaguzi huo unaangaziwa kuwa muhimu unaoweza kubadili mustakabali wa Afrika Kusini, mwanachama muhimu wa umoja wa nchi zinazoibukia kiuchumi na zinazoendelea duniani, zinatambulika kwa pamoja kama Global South.

Vituo vya kupigia kura vilifungwa saa tatu usiku kwa saa za nchi hiyo jana Jumatano. Zoezi la kuhesabu kura linatarajiwa kutumia siku kadhaa.