Japani kutoa msaada wa reli nchini Ukraine ili kusaidia ujenzi mpya wa mtandao wa usafiri

Japani inatoa msaada wa reli nchini Ukraine ili kusaidia ujenzi mpya wa mtandao wake wa reli ulioharibiwa vibaya na uvamizi wa Urusi.

Hafla ya makabidhiano ilifanyika jijini Kyiv jana Jumanne. Miongoni mwa wahudhuriaji ni pamoja na Balozi wa Japani Matsuda Kuninori na maafisa wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani.

JICA itatoa reli za tani 25,000 ambazo ni sawa na urefu wa takribani kilomita 190. Hizo zitasafirishwa kutoka Japani hadi Poland kwa meli, kisha kuwasilishwa nchini humo kwa njia ya reli. Awamu ya kwanza ya msaada huo tayari imewasili.

Mashine za kunyanyulia vitu vizito na vifaa vingine pia vitatolewa katika msaada huo.

Ukraine inapata ugumu wa kupata reli ndani ya nchi hiyo baada ya kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mji wa Mariupol mashariki mwa nchi hiyo kuharibiwa na vikosi vya Urusi.

Mkuu wa kampuni ya reli inayomilikiwa na serikali, Yevhen Liashchenko aliuita msaada huo wa Japani kuwa ni muhimu, akiongeza kuwa “reli ni damu” ya miundombinu ya Ukraine.