Televisheni inayoendeshwa na serikali ya China imerusha mazoezi ya kijeshi yaliyohusisha roboti mbwa na droni zenye akili mnemba, AI

Televisheni inayoendeshwa na serikali ya China, China Central Television, au CCTV imerusha picha za video zinazoonesha mazoezi ya kijeshi yanayohusisha roboti mbwa na droni zenye teknolojia ya akili mnemba, au AI.

Televisheni hiyo iliripoti kuhusu mazoezi ya pamoja na Cambodia ambayo yamekuwa yakiendelea katika nchi hiyo iliyopo Kusini mashariki mwa Asia tangu Mei 16.

CCTV inasema roboti mbwa inayoendeshwa kutoka mbali inaweza kutembea, kuruka, kulala chini na kutuma picha za muda halisi za uchunguzi.

Roboti kubwa zaidi ya mbwa, yenye uzito wa kilo 50, inaweza kufyatua risasi kutoka kwenye bunduki iliyowekwa mgongoni mwake. Picha hiyo ya video inaonesha roboti ikiwaongoza wanajeshi kuelekea ndani ya jengo moja.

Droni zenye teknolojia ya AI zinaonekana zikifyatua risasi kutoka angani.

Jeshi la Marekani limekuwa likitumia roboti mbwa na droni zenye uwezo wa AI katika mazoezi.

China inaaminika kuonesha kuwa jeshi lake linaongeza uwezo wake kwa teknolojia ya kisasa.