Hong Kong yawakamata watu 6 kutokana na machapisho kwenye Facebook ya mikesha ya uwanja wa Tiananmen

Polisi katika eneo la Hong Kong wanasema wamewakamata watu sita kwa tuhuma za kukiuka sheria mpya ya usalama wa taifa kwa kutuma jumbe za uchochezi kwenye mtandao wa Facebook na kuchochea chuki dhidi ya mamlaka.

Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kuwa hawa ni watu wa kwanza kukamatwa chini ya sheria ambayo ilianza mwezi Machi.

Sita waliokamatwa jana Jumanne ni pamoja na Chow Hang Tung, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa kikundi kilichokuwa kikiandaa mikesha ya kila mwaka ya kuwakumbuka waathirika wa msako wa Uwanja wa Tiananmen mnamo Juni 4, mwaka 1989.

Ukurasa wa Facebook unaozungumziwa unaangazia machapisho kuhusu mikesha ya zamani.

Polisi wanasema washukiwa walilenga "tarehe nyeti inayokuja," inaonekana wakirejelea kumbukumbu ya tukio hilo.

Pia wanatoa hoja kuwa machapisho hayo yalilenga kuibua chuki dhidi ya serikali kuu na ile ya Hong Kong na kuwachochea watumiaji wa mtandao huo kupanga au kushiriki katika shughuli haramu.