Mvua kubwa yatarajiwa kunyesha maeneo ya Kyushu, Shikoku na Tokai

Maeneo ya magharibi mwa Japani na maeneo mengine yanashuhudia mvua kubwa iliyotokana na hewa ya joto na yenye unyevunyevu inayoelekea kwenye mfumo wenye mgandamizo mdogo wa hewa juu ya kusini mwa Kyushu.

Mvua kubwa za kimaeneo na mvua za radi zinatarajiwa kunyesha huko Okinawa, Amami na magharibi mwa Japani leo Jumanne, na hadi kesho Jumatano katika eneo la Tohoku na mashariki mwa Japani.

Watabiri wa hali ya hewa pia wanasema makundi ya mawingu mazito ya mvua yanaweza yakajiunda na kusababisha mvua kubwa katika mikoa ya Kochi na Tokushima hadi leo jioni.

Makundi sawia ya mawingu mazito ya mvua yanaweza kuathiri mikoa ya Aichi, Gifu na Shizuoka hadi usiku. Aina hii ya mvua kubwa inaweza kuongeza hatari ya janga katika muda mfupi.

Maafisa wa hali ya hewa wanatoa tahadhari ya kutokea kwa maporomoko ya udongo, mafuriko katika maeneo ya mabonde, kufurika kwa mito pamoja na radi, dhoruba, pepo kali na mvua ya mawe.

Pia wanatoa wito kwa watu kukaa kwenye majengo imara ikiwa wataona dalili za mawingu ya mvua ya radi yaliyojiunda yakikaribia.