Maswali na Majibu: Ajali za bidhaa za kawaida katika msimu wa mvua na joto (2)

(2) Moto unaotokana na vumbi linaloweza kusababisha mzunguko mdogo wa umeme

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Matumizi mabaya ya vifaa vya umeme yanaweza kusababisha matatizo yasiyotarajiwa, na baadhi ya ajali hutokea mara kwa mara katika msimu fulani kuliko nyakati zingine za mwaka. Mfululizo huu unaangazia ajali za bidhaa ambazo hutokea mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua na joto. Kipengele cha hii leo kinaangazia mioto inayosababishwa na mzunguko mdogo wa umeme.

Tukio la moto uliosababishwa na mzunguko mdogo wa umeme linamaanisha mchakato ambapo vumbi linalojikusanya mahali fulani kati ya plagi ya umeme na sehemu ya kutolea umeme huwa na unyevu, na kutengeneza hali nzuri ya kupitisha umeme ambayo inaweza ikasababisha moto kuzuka. Ni muhimu kuwa makini katika msimu ambapo hali ya unyevu huonekana kuongezeka kutokana na mvua.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Idara ya Zimamoto ya Tokyo, katika kipindi cha miaka 10 hadi mwaka 2022, visa 170 vya moto wa aina hiyo viliripotiwa katika makazi ya Tokyo.

Taasisi ya Taifa ya Teknolojia na Tathmini (NITE) inapendekeza kuchukuliwa kwa hatua zifuatazo ili kuzuia kuzuka kwa mioto kama hiyo. Zinajumuisha kusafisha mara kwa mara maeneo yaliyo karibu na plagi ya umeme na ya sehemu ya kutolea umeme, kuchomoa kamba ya umeme iwapo kifaa hakitatumiwa kwa muda mrefu, na kufuatilia kukusanyika kwa unyevu kwenye au karibu na sehemu ya kutolea umeme na plagi. Iwapo cheche ama moshi utatokea jirani na sehemu ya kutolea umeme, chomoa haraka kamba ya umeme ama zima swichi ya umeme.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 28, 2024.