Nchi ndogo za visiwa zataka fedha zaidi kupambana na janga la tabia nchi

Nchi ndogo za visiwa zimetoa wito kwa nchi zenye utajiri mkubwa kutoa fedha zaidi ili kuzisaidia kukabiliana na matishio yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi. Wito huo ulitolewa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, UN ulioanza jana Jumatatu.

Mkutano wa Kimataifa wa Nchi Ndogo Zinazoendelea za Visiwa hufanyika mara moja katika kipindi cha mwongo mmoja. Nchi kutoka visiwa vya Caribbean ya Antigua na Barbuda ndio mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu unaohudhuriwa na takribani nchi 100 ikiwemo Japani.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres aliyaita mabadiliko ya tabia nchi kuwa “janga lililopo kwa familia yote ya binadamu.” Lakini aliongezea kuwa, nchi ndogo zinazoendelea za visiwa zipo kwenye mistari ya mbele ya janga la tabia nchi. Alisisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuzisaidia nchi hizo.

Waziri Mkuu wa Taifa Huru la Samoa alizisihi nchi zilizoendelea kiviwanda kutoa fedha zaidi na aina zingine za msaada.

Mkutano huo unatarajiwa kumalizika Alhamisi wiki hii. Washiriki wanatarajiwa kuidhinisha mpango wa hatua za kuchukuliwa mwongo ujao.