Shambulizi la anga mjini Rafah laua watu wasiopungua 45

Maafisa wa afya katika eneo la Gaza wanasema shambulizi la anga la Israel mjini Rafah juzi Jumapili limeua watu wasiopungua 45. Picha za video zilizochukuliwa na NHK katika eneo la tukio zinaonyesha mahema yaliyoharibiwa kabisa.

Shambulizi hilo la vikosi vya Israel limekuja baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ kutoa hatua za muda zilizoiagiza Israel kusitisha mara moja mashambulizi yake mjini Rafah.

Mwanamume mmoja anayeishi jirani na mji huo alisema aliwaona waathiriwa wakiwa wamelala ardhini, na kwamba walikuwa ni wanawake, watoto na wazee.

Jeshi la Israel lilisisitiza kwamba shambulizi hilo liliwalenga wanachama wawili waandamizi wa Hamas. Liliongeza kuwa hatua kadhaa zilichukuliwa kupunguza hatari ya vifo vya raia.

Serikali ya Israel ilisema taarifa za awali zinaashiria kuwa moto ulizuka baada ya shambulizi hilo ambao unaonekana kusababisha vifo vya raia.

Serikali hiyo pia ilisema vifo vya raia ni jambo la kusikitisha, “lakini hivi ni vita ambavyo Hamas ilivitaka na kuvianzisha.”