Serikali ya Japani kuendelea kujihadhari baada ya Korea Kaskazini kushindwa kurusha satelaiti

Serikali ya Japani itaendelea kuchukua tahadhari kufuatia uwezekano wa Korea Kaskazini kurusha satelaiti.

Korea Kaskazini ilisema kuwa jaribio lake la hivi karibuni lililofanyika jana Jumatatu la kurusha satelaiti ya upelelezi wa kijeshi lilishindikana baada ya roketi iliyobeba satelaiti hiyo kulipuka wakati wa hatua ya kwanza ya kuruka.

Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Japani Hayashi Yoshimasa alishutumu urushaji huo.

Alisema urushaji huo unakiuka maazimio husika ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ni suala nyeti linalohusu usalama wa watu wa Japani.

Serikali ya Japani inapanga kuendelea kuchukua hatua za kujiandaa kwa uchokozi zaidi. Hatua hizo ni pamoja na kuendelea kutumika kwa mitambo ya PAC-3 ya kudungua makombora katika visiwa vya Sakishima mkoani Okinawa.

Taarifa ya muda wa kurusha roketi iliyotolewa na Korea Kaskazini itadumu hadi Juni 3 mwaka huu.