Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani aisihi Israel kuheshimu agizo la ICJ kusitisha mashambulizi mjini Rafah

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Kamikiwa Yoko ameisihi Israel kuheshimu agizo la Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ la kusitisha operesheni zake za kijeshi mjini Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kamikawa alizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz kwa njia ya simu jana Jumatatu.

Ijumaa iliyopita, ICJ ilitoa hatua za muda na kuiagiza Israel kusitisha mara moja mashambulizi yake ya kijeshi mjini Rafah na kuuacha wazi mpaka wa Rafah kwa ajili ya msaada wa kibinadamu. Lakini jeshi la Israel limeendelea na mashambulizi yake.

Kamikawa alisema serikali ya Japani ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza na inapinga operesheni kamili ya kijeshi mjini Rafah.

Aliongeza kuwa agizo la ICJ linapaswa kufuatwa kisheria na pande zote katika mzozo na linapaswa kutekelezwa kwa nia njema.

Katz aliripotiwa kuelezea msimamo wa nchi yake.