Viongozi wa Japani, China na Korea Kusini wafanya mkutano wa pamoja wa wanahabari

Viongozi wa Japani, China na Korea Kusini wamekutana kwa mazungumzo jijini Seoul nchini Korea Kusini. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa nchi hizo tatu kufanya mkutano wa pande tatu katika kipindi cha miaka minne na nusu.

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio, Waziri Mkuu wa China Li Qiang na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol wamekutana leo Jumatatu asubuhi.

Viongozi hao watatu wamejadili mpango wa Korea Kaskazini wa hivi karibuni wa kurusha kile inachokiita satelaiti kufuatia taarifa iliyotolewa na Korea Kaskazini.

Walitoa taarifa ya pamoja yenye kuelezea mazungumzo yao kwa kifupi.

Baada ya mkutano huo, Yoon alisema mpango wa Korea Kaskazini wa kurusha kile inachokiita satelaiti ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuichukulia hatua thabiti Korea Kaskazini.

Alisema taarifa yao ya pamoja inajumuisha azimio la nchi hizo tatu kushirikiana kwa karibu kwa ajili ya amani na ustawi wa eneo hilo.