Maswali na Majibu: Ajali za bidhaa za kawaida wakati wa msimu wa mvua na joto (1)

(1) Kufua nguo zisizopenyesha maji

NHK inajibu maswali kuhusu kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya umeme vya majumbani yanaweza kusababisha tatizo lisilotarajiwa, na baadhi ya ajali hutokea mara kwa mara katika msimu fulani kuliko kipindi kingine cha mwaka. Mfululizo huu unaangazia ajali zitokanazo na bidhaa ambapo hutokea mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua na msimu wa joto. Katika makala ya leo tutazungumzia mtikisiko usio wa kawaida wa mashine ya kufulia unaosababishwa na nguo zisizopenyesha maji.

Taasisi ya Taifa ya Teknolojia na Tathmini (NITE) imeibua tahadhari dhidi ya kufua na kukausha kwa kuzungusha koti la mvua na nguo zingine zisizopenyesha maji katika mashine ya kufulia, ikisema mtikisiko usio wa kawaida unaweza kusababisha ajali. Wakati kitambaa kisichopenyesha maji kinapowekwa kwenye mashine ya kufulia, maji yatakwama katika matabaka ya nguo. Ikiwa ikikaushwa kwa kuzungushwa katika hali hiyo, beseni litakosa uwiano. Katika kesi nyingi, ufanyaji kazi salama wa mashine utabaini tatizo na kuacha kuzunguka, lakini ni muhimu kuwa makini kwamba ajali zinaweza kutokea ikiwa uwiano wa beseni umetatizwa wakati wa uzungukaji wa kasi kubwa.

Kama mzunguko utaendelea katika hali isiyo ya uwiano, nguo zinaweza kurushwa nje ya beseni, mashine au kuta na sakafu kuzunguka mashine zinaweza kuharibiwa. Katika baadhi ya visa, mashine ya kufulia huanguka. Ili kuepuka tatizo kama hilo, NITE inaonya dhidi ya kufua nguo zisizopenyesha maji. Mifano ya nguo zisizopenyesha maji mbali na makoti ya mvua ni suti za kuogelea, nguo za kutelezea kwenye theluji na mikeka ya plastiki. Kwa mujibu wa NITE, unaweza kuangalia ikiwa nguo haipitishi maji au la kwa kugusisha mdomo wako na kuipulizia hewa. Ikiwa hewa haipenyi, basi haipitishi maji.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 27, 2024.