Tamko la pamoja laidhinishwa katika mkutano wa pande tatu wa viongozi wakuu wa Japani, China na Korea Kusini

Viongozi wa Japani, China na Korea Kusini wameidhinisha tamko la pamoja linalojumuisha ahadi zao za kuendelea na juhudi chanya kwa ajili ya suluhisho la kisiasa kwa suala la Rasi ya Korea.

Mkutano wa pande tatu kati ya Mawaziri Wakuu Kishida Fumio wa Japani na Li Qiang wa China na Rais Yoon Suk-yeol wa Korea Kusini ulifanyika mjini Seoul jana Jumatatu.

Tamko hilo linasema kuwa viongozi hao walithibitisha tena kujitolea kwao kwa malengo na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na utaratibu wa kimataifa wa kuzingatia utawala wa sheria na sheria za kimataifa.

Pia linasena viongozi hao walikubaliana kwamba mkutano wa pande tatu wa viongozi wakuu wa nchi hizo na mkutano wa pande tatu wa Mawaziri wa Mambo ya Nje inapaswa kufanyika mara kwa mara bila mapumziko.

Tamko hilo linasema kuwa nchi hizo tatu zitatenga mwaka 2025-2026 kama Mwaka wa Mabadilishano ya Kitamaduni miongoni mwa nchi hizo tatu, huku pia zikitafuta kuongeza idadi ya mabadilishano ya pande tatu ya watu hadi milioni 40 kufikia mwaka 2030 kupitia utalii na nyanja zingine.

Viongozi hao pia walikubaliana kudumisha majadiliano kwa ajili ya kuharakisha makubaliano huru ya kibiashara ya pande tatu kwa lengo la kufikia makubaliano huru ya kibiashara yenye manufaa kwa pande zote tatu, yenye uhuru, usawa, wigo mpana na thamani ya juu.