EU yaitaka Israel kukubali amri ya ICJ ya kusitisha mashambulizi Rafah

Mkuu wa sera ya kigeni ya Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameitaka Israel kumaliza operesheni zake za kijeshi mjini Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza, akisema mashambulizi hayo yapo kinyume cha uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ.

Katika mkutano na wanahabari jana Jumapili mwakilishi huyo mkuu wa Umoja wa Ulaya alisema kuwa mipaka muhimu bado imefungwa kwa usambazaji wa misaada Gaza. Amesema “hilo limetokea kinyume cha uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa - - Mahakama ya Kimataifa ya Haki.”

Borrell ameongeza kwamba amri hiyo “ni lazima ifuatwe na itekelezwe vilivyo na kikamilifu.”

Akizungumzia shambulizi la roketi la Hamas dhidi ya Israel jana Jumapili, Borrell alisema “hilo pia linapaswa kukoma.” Amesisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa lazima ifanye kila kitu ili kufanikisha usitishaji vita, uachiliwaji wa mateka, na uboreshaji wa hali ya kibinadamu Gaza.

Ijumaa iliyopita ICJ ilikabidhi hatua za muda zinazoitaka
Israel kusitisha mara moja mashambulizi yake mjini Rafah na kufungua vituo vya ukaguzi ili kuruhusu msaada mkubwa wa kibinadamu. Imesema hali ya Gaza inaendelea kuzorota.