Mkuu wa zamani wa ASDF: Inayodaiwa kuwa satelaiti ya Korea Kaskazini inaonekana ni ya ufuatiliaji wa kambi za Marekani

Mkuu wa zamani wa Kikosi cha Kujihami cha Anga cha Japani, ASDF, Kataoka Haruhiko amesema kile ambacho Korea Kaskazini inadai kuwa satelaiti ya upelelezi wa kijeshi inaonekana imekusudiwa kufuatilia kambi za Marekani. Mwaka jana, Korea Kaskazini ilisema imefanikiwa kurusha kitu hicho.

Kataoka, ambaye kwa sasa anafanya kazi katika Taasisi ya Japani ya Anga za Juu na Usalama, amesema mzunguko wa chombo hicho ni karibu sawa na satelaiti za ukusanyaji taarifa za Japani.

Kataoka ameashiria kwamba ni satelaiti ambayo imekusudiwa kupiga picha za uso wa dunia. Lakini amesema bila uchambuzi zaidi, haiwezekani kujua namna picha hizo zinavyoonekana vizuri na ikiwa satelaiti hiyo imefanikiwa kutuma picha duniani.

Kataoka pia amerejelea tangazo la Korea Kaskazini kwamba inapanga kurusha satelaiti tatu zaidi za upelelezi wa kijeshi mwaka huu.

Amesema Korea Kaskazini pengine itarusha satelaiti kama ilivyopangwa na inatarajiwa kufanya urushaji zaidi katika mwaka ujao wa fedha na kuendelea, kutokana na uwezo ulioongezeka wa uendelezaji.