Tel Aviv yalengwa na shambulio la roketi la Hamas huku Israel ikiendelea na mashambulizi Rafah

Tel Aviv imeshambuliwa kwa roketi ya Hamas huku Israel ikiendelea na mashambulizi yake mjini Rafah, kusini mwa Gaza. Vyombo vya habari vya Israel vinasema Tel Aviv ililengwa kwa mara ya kwanza tangu mwezi Januari.

Jeshi la Israel limesema kuwa limewaua "magaidi" waliojaribu kuwashambulia wanajeshi wake Rafah. Jeshi hilo pia limesema askari hao walikuta silaha nyingi, kama vile bunduki.

Maafisa wa afya wa Gaza wanasema watu 35, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa katika shambulio la bomu la Israel kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao kaskazini magharibi mwa Rafah Jumapili jioni.

Shirika la Habari la CNN lilimnukuu afisa mmoja wa Misri akisema mazungumzo kati ya Israel na Hamas kwa ajili ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka yataanza tena kesho Jumanne jijini Cairo, Misri.

Lakini mtazamo wa makubaliano yoyote bado hauko wazi kwani kuna hali kubwa ya kutofautiana kati ya pande hizo mbili.