Korea Kaskazini inapanga kurusha 'satelaiti'

Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha Japani kinasema kuwa kimefahamishwa na Korea Kaskazini kuhusu mpango wake wa kurusha kile inachokiita satelaiti katika kipindi kati ya Mei 27 na Juni 3.

Kifaa hicho huenda kikaangukia katika mojawapo ya maeneo matatu -- maeneo mawili katika Bahari ya Njano kusini magharibi ya Korea Kaskazini na moja katika Bahari ya Pasifiki mashariki ya Ufilipino. Maeneo yote hayo yapo nje ya ukanda maalum wa kiuchumi wa Japani.

Maafisa wanavitaka vyombo vinavyofanya kazi majini kuchukua tahadhari kwa vitu vyovyote vinavyoanguka kutoka juu.

Kikosi kazi cha serikali ya Japani katika ofisi ya waziri mkuu kinakusanya na kuchunguza taarifa hizo.

Waziri Mkuu Kishida Fumio ameziagiza wizara na taasisi husika kuwapatia watu taarifa stahiki kwa kukusanya na kufanya uchunguzi wa kina wa taarifa za kiintelijensia.