Mazungumzo ya pande mbili yafanyika kabla ya mkutano wa Japani, China na Korea Kusini

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio amefanya mazungumzo na viongozi kutoka China na Korea Kusini kwa nyakati tofauti jijini Seoul.

Mikutano hiyo ya jana Jumapili imefanyika siku moja kabla ya mkutano wa kwanza wa pande tatu wa nchi hizo jirani za Asia katika kipindi cha miaka zaidi ya minne.

Kishida kwanza alikutana na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol. Wamekubaliana kuboresha zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili kabla ya kutimiza miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia mwakani 2025.

Viongozi hao pia waliijadili Korea Kaskazini. Nchi hiyo imekuwa ikiongeza uendelezaji wake wa silaha za nyuklia na makombora.

Kadhalika Kishida alikutana na Waziri Mkuu wa China Li Qiang.

Wawili hao walisisitiza kukuza “uhusiano wenye manufaa wa pande mbili kulingana na maslahi ya pamoja ya kimkakati.” Kitu alichokubaliana Kishida na Rais Xi Jinping mwezi Novemba mwaka jana.