Israel yaendelea na mashambulizi huko Rafah licha ya agizo la ICJ la kusitisha mara moja

Vikosi vya Israel vimeendelea kufanya mashambulizi huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza licha ya Mahakama Kuu ya Kimataifa, ICJ kuiamuru nchi hiyo kusitisha mara moja mashambulizi yake hapo.

Israel ilitangaza mahala ilipofanya oparesheni yake ya kijeshi huko Gaza juzi Ijumaa. Siku hiyo mahakama ya ICJ iliyopo mjini The Hague ilitoa hatua yenye masharti.

Israel ilisema vikosi vyake vilivunja kiini cha magaidi huko Rafah, na kuyaondoa makumi ya wapiganaji wake huko Jabalia kaskazini mwa Gaza.

Wakati huo huo, maafisa wa afya huko Gaza walisema jana Jumamosi kwamba walithibitisha vifo 46 kwenye ukanda huo katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Walisema idadi ya vifo tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel mnamo Oktoba 7 vimeongezeka hadi 35,903.

Baadhi ya vyombo vya habari vimewanukuu maafisa wakisema majadiliano yaliyokwama kwa ajili ya kusitisha mapigano, na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa huko Gaza, yanatarajiwa kurejea katika siku zijazo.

Shirika la habari la Reuters lilimnukuu afisa akizungumzia kuhusu uamuzi wa kuanza tena majadiliano baada ya mkuu wa shirika la kijasusi la Israel, Mossad kukutana na mkuu wa CIA na waziri mkuu wa Qatar.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa majadiliano "yatafungua mapendekezo mapya yatakayoongozwa na wapatanishi, Misri na Qatar," na ushiriki wa karibu wa Marekani.

Israel na Hamas zimeheshimu kusitisha mapigano mara moja tu tangu mgogoro huo ulipoanza Oktoba 7. Usitishaji huo ulidumu kwa siku saba tu kuanzia mwishoni mwa Novemba mwaka jana. Lakini pande zote zimesalia katika uhasama, hivyo kukwamisha makubaliano ya usitishaji mwingine.

Bado haijawa wazi iwapo mkwamo huo unaweza kutatuliwa, hata kama majadiliano yatarejea.