Wakuu wa fedha wa G7 waelezea wasiwasi kuhusu uzalishaji uliozidi wa viwandani wa China

Wakuu wa fedha na magavana wa benki kuu wa Kundi la nchi Saba zenye viwanda vingi duniani G7 wameelezea wasiwasi kuhusu uzalishaji uliozidi wa viwandani nchini China.

China inatuhumiwa kutengeneza magari mengi kupita kiasi ya umeme na bidhaa zingine ili kuziuza nje ya nchi katika bei ndogo isiyokuwa na usawa.

Maafisa wa G7 walitoa taarifa ya pamoja baada ya kuhitimisha mkutano wa siku mbili katika mji wa Stresa, kaskazini mwa Italia jana Jumamosi.

Taarifa hiyo ilisema, “Tunaelezea wasiwasi kuhusiana na matumizi ya wigo mpana ya China kwenye sera na vitendo visivyokuwa vya kimasoko ambavyo vinadhoofisha ustahamilivu wa wafanyakazi, viwanda na uchumi wetu.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa maafisa hao “watafikiria kuchukua hatua za kuhakikisha kunakuwa na usawa, unaokwenda sambamba na kanuni za Shirika la Kimataifa la Biashara.”

Washiriki pia walijadili wazo la kuisaidia Ukraine kwa kutumia faida inayotoka kwenye mali za Urusi ambazo zimezuiwa kama sehemu ya vikwazo juu ya nchi hiyo kuivamia Ukraine.

Taarifa hiyo ilisema maafisa wanadhamiria kuwasilisha chaguo kwa viongozi wao kabla ya mkutano wa viongozi wakuu wa G7 utakaofanyika mwezi ujao.

Waziri wa Fedha wa Japani Suzuki Shunichi alizungumza na wanahabari ambapo alisema msimamo wa awali wa nchi yake ni kwamba sheria ya kimataifa lazima ifuatwe, kuhusiana na matumizi ya faida za mali za Urusi, kwa sababu nchi hiyo inalalamikiwa kwa vitendo vyake vya kukiuka sheria ya kimataifa.

Maafisa wa G7 bado wamegawanyika juu ya namna ya kushughulika na mali za Urusi. Bado haijafahamika ni kwa kiasi gani wataweza kupunguza ombwe katika mkutano wa viongozi wakuu wa G7.