Kishida atembelea jijini Seoul kwa mkutano wa viongozi wakuu wa China na Korea Kusini

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio aliondoka kwenda jijini Seoul leo Jumapili ili kukutana na Waziri Mkuu wa China Li Qiang na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol. Utakuwa ni mkutano wa kwanza wa viongozi wakuu wa mataifa hayo matatu katika kipindi cha miaka minne na nusu. Mipango inaendelea ya kufanikisha mkutano wa pande mbili kati ya Kishida na Li.

Viongozi hao watatu watafanya mkutano katika mji mkuu wa Korea Kusini Seoul kesho Jumatatu. Wanaonekana huenda wakathibitisha kufanikisha zaidi mabadilishano ya watu kupitia mwingiliano wa kimataifa wa vyuo na utalii. Huenda pia wakauchagua mwaka 2025 na 2026 kuwa ni mwaka wa mabadilishano ya kitamaduni.

Kabla ya mkutano huo, leo Jumapili Kishida amepangiwa kufanya mkutano wa pande mbili na Yoon. Huenda watakubaliana kuwa na mawasiliano ya karibu kati ya viongozi hao na mawaziri.

Viongozi hao wawili pia wanatarajiwa kutafuta kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na Korea Kaskazini, ambayo imekuwa ikiongeza mipango yake ya silaha za nyuklia na makombora.

Kishida pia anapanga mkutano wa pande mbili na Li. Waziri mkuu huyo wa Japani anaonekana kuwa na shauku ya kuthibitisha tena nia yao ya kukuza “uhusiano wa pamoja wenye tija kulingana na maslahi ya kimkakati ya pamoja.”

Kishida huenda atatafuta uondolewaji mara moja wa katazo la China kwenye bidhaa za vyakula vya baharini vya Japani vinavyonunuliwa nchini China na kuainisha msimamo wa serikali yake juu ya masuala mengine ya pande mbili ambayo hayajatatuliwa.

Kishida pia anatarajiwa kutoa wito kwa China ili kutatua kwa amani masuala yanayohusiana na Taiwan kupitia mazungumzo.