Putin na Lukashenko wajadili mazoezi ya silaha za nyuklia

Rais wa Urusi Vladimir Putin anaahidi ushirikiano zaidi na mshirika muhimu. Juzi Alhamisi na jana Ijumaa Putin alikutana na Rais wa Belarusi Alexander Lukashenko jijini Minsk nchini Belarusi kujadili uhusiano wa kiuchumi na mazoezi ya pamoja ya silaha za nyuklia.

Mapema wiki hii, vikosi vya Urusi vilianza kile wanachokiita "mafunzo ya vitendo" na silaha zao za kimkakati za nyuklia. Putin alisema zoezi hilo litahusisha hatua tatu, na Belarusi yenye silaha za nyuklia za Urusi zilizohifadhiwa katika eneo lake itajiunga na hatua ya pili.

Putin alielezea mazoezi hayo kama "yaliyopangwa na ya kawaida" na akasema Urusi na Belarusi "hazichochei chochote." Aliongeza kuwa nchi hizo mbili zinahitaji kuratibu kwa sababu haziwezi kuruhusu "kutofaulu" au "makosa," na akadokeza kuwa wanachama wa NATO hufanya mazoezi kama hayo.

Lukashenko alisema Belarus na Urusi "hazina nia ya kumshambulia yeyote" lakini lazima ziwe na uwezo wa kutumia silaha "kujilinda" zenyewe.

Pia alisema nchi hizo mbili zitalindana zenyewe dhidi ya mataifa ya Magharibi ambayo yamewawekea vikwazo. Aliongeza kuwa lazima "wakamilishe mara moja" sera ya umoja ya viwanda.