ICJ yaiagiza Israel kusitisha oparesheni yake katika eneo la Rafah

Kwa mara ya kwanza Mahakama Kuu ya Kimataifa, ICJ imetoa wito kwa Israel kusitisha oparesheni yake ya kijeshi katika mgogoro wake na Hamas. Jana Ijumaa, imewasilisha kile kinachofahamika kama hatua yenye masharti “kusimamisha mara moja” mashambulizi katika eneo la Rafah.

Majaji katika mahakama mjini The Hague nchini Uholanzi wanasema mapigano yamesababisha hali za kibinadamu walizoziita “balaa.”

Rais wa ICJ, Nawaf Salam, alisema hali iliyotokana na mashambulizi ya Rafah inaleta hatari zaidi ya madhara “yasiyoweza kurekebishwa” ya haki kwa Wapalestina.

Hapo awali majaji waliiagiza Israel kuchukua hatua zote stahiki kuzuia mauaji ya halaiki ya raia na kuhakikisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu. Hata hivyo, hawajathibitishwa kwamba juhudi hizo zimekuwa za kutosha.

Raia wengi wamekuwa wakiripotiwa mara kwa mara kulazimishwa kuhama wakati wa mashambulizi katika eneo la Rafah, hivyo majaji wanaomba hatua zaidi, ikiwemo kuhakikisha kwamba mpaka wa Rafah unasalia kuwa wazi kwa “kutozuiliwa” misaada ya kibinadamu.