Marekani na Misri zakubaliana kurejesha uwasilishaji wa misaada Gaza kupitia mpaka wa ardhini

Marekani na Misri zimekubaliana kurejesha uwasilishaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza kupitia mpaka wa ardhini.

Ikulu ya Marekani imesema Rais Joe Biden alizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi juzi Ijumaa.

Iligusia kuwa Biden alifurahia dhamira ya Sisi ya kuruhusu usambazaji wa misaada ya kibinadamu inayotolewa na UN kutoka Misri kupitia mpaka wa Kerem Shalom kwa muda. Upande wa Misri pia ulitangaza makubaliano hayo.

Hatua hiyo inakuja wakati huu kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula katika eneo la Gaza.

Umoja wa Mataifa, UN umesema mpaka wa Rafah kati ya Misri na kusini mwa Gaza umefungwa tangu jeshi la Israel lianze oparesheni ya ardhini.

Uwasilishaji wa misaada kupitia gati iliyojengwa kwa muda na Marekani kwenye pwani ya Gaza ulianza Mei 17.

Wizara ya Ulionzi ya Marekani ilisema Alhamisi iliyopita kwamba tani 506 za msaada zimesambazwa na UN huko Gaza tangu jitihada hizo zilipoanza.

Lakini gazeti la Marekani la Wall Street Journal limesema kiwango cha misaada hiyo kinakadiriwa kuwa sawa na malori 71, ambayo ni kiwango cha chini zaidi ya lengo la awali la kuwa na malori 90 kwa siku.

Gazeti hilo pia limesema kiwango hicho ni takribani asilimia 15 ya makadirio ya chini ya kila siku yanayohitajika kwa ajili ya watu zaidi ya milioni mbili.