Wapiga kura wa New Delhi wapiga kura katika awamu ya hivi karibuni ya uchaguzi mkuu wa India

Wapiga kura katika mji mkuu wa India, New Delhi wamepiga kura zao katika awamu ya sita ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Awamu ya sita kati ya saba za uchaguzi ilifanyika jana Jumamosi. Awamu ya kwanza ilifanyika Aprili 19 na ya mwisho itafanyika Juni Mosi. Jumla ya viti 543 vinawaniwa.

Waziri Mkuu Narendra Modi, anayetokea chama tawala cha Bharatiya Janata, anatafuta kutawala katika awamu ya tatu. Muungano wa vyama vya upinzani unaotokana na chama cha Indian National Congress unalenga kushika hatamu ya serikali.

New Delhi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uchafuzi wa hali ya hewa na msongamano wa magari.

Mji huo mkuu pia unakabiliwa na mawimbi ya hewa ya joto, huku hali hiyo ikizidi nyuzijoto 40 za Selisiyasi.

Uhaba wa maji pia ni tatizo lingine kubwa kwenye vitongoji masikini vinavyokabiliwa na ukosefu wa maji.

Uamuzi wa wapiga kura wa New Delhi katika masuala haya unavutia nadhari, kwa sababu ushindi wa viti katika mji huo mkuu ni muhimu kwa pande zote za chama tawala na kambi ya upinzani.

Zoezi la kuhesabu kura litafanyika kote nchini humo mnamo Juni 4.