Msalaba warejeshwa katika kanisa la Notre-Dame jijini Paris

Msalaba juu ya kanisa la Notre-Dame jijini Paris umerejeshwa miaka mitano baada ya kutokea moto mkubwa.

Moto wa mwaka 2019 ulisababisha madhara makubwa katika mnara na paa la kanisa hilo.

Msalaba wenye urefu wa mita 12 ilikuwa ni kazi ya uhunzi iliyobuniwa na msanifu majengo maarufu katika karne ya 19. Msalaba huo uliharibiwa wakati mapambo yake yalipopotea katika janga hilo.

Wahunzi na wafanyakazi wamekamilisha urejeshaji wa msalaba huo.

Juzi Ijumaa, msalaba uliorejeshwa uliwekwa katika sehemu yake kwa winchi baada ya maombi kutolewa na mchungaji.

Watu katika tukio hilo walishangilia msalaba huo ulipowekwa mahali pake juu ya muundo wa kanisa hilo takribani mita 40 juu ya ardhi.

Mnara pia umerejeshwa wakati juhudi za ujenzi mpya zimekuwa zikiongezeka kabla ya muda uliopangwa wa kulifungua tena kanisa hilo kwa umma mnamo Disemba 8.

Philippe Jost, ambaye anasimamia mradi wa ujenzi mpya, alisema kwamba watu watakaokuja Paris kwa ajili ya Mashindano ya Olimpiki mwezi Julai, wataweza kuona “kanisa zuri” kabla ya kufunguliwa tena.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vinaripoti kuwa kanisa la Notre-Dame de Paris huenda likawa sehemu ya sherehe za ufunguzi za Olimpiki ambazo zitafanyika katika Mto Seine.