Mawaziri wa ulinzi wa Japani, Korea Kusini watarajiwa kujadili kurejelea mabadilishano

Mawaziri wa ulinzi wa Japani na Korea Kusini wanatarajiwa kujadili kurejesha mabadilishano kati ya Vikosi vya Kujihami vya Japani, SDF na jeshi la Korea Kusini.

Vyanzo vya habari katika serikali ya Japani vinasema kwamba uratibu unaendelea kwa ajili ya mkutano wa Waziri wa Ulinzi wa Japani Kihara Minoru na mwenzake wa Korea Kusini Shin Won-sik pembezoni mwa Majadiliano ya Shangri-La, yatakayoanza Mei 31 nchini Singapore.

Mabadilishano baina ya SDF na jeshi la Korea Kusini yalikuwa yamesitishwa kufuatia tukio la rada mwaka 2018.

Serikali ya Japani inasema manowari ya Jeshi la Majini la Korea Kusini iliielekeza rada ya udhibiti moto kwenye ndege ya doria ya SDF katika Bahari ya Japani. Lakini Korea Kusini inasema meli yake haikuielekeza rada yake kuilenga ndege.

Kufutia kuimarika kwa uhusiano wa pande mbili, mawaziri wa ulinzi wa Japani na Korea Kusini walikubaliana mwaka jana kuharakisha majadiliano kuhusiana na suala hilo ikiwemo hatua za kuzuia matukio kama hayo.

Kihara na Shin hawatarajiwi kuwa na majadiliano ya kina juu ya tukio la rada, kutokana na pande hizo mbili kuwa na tofauti juu ya suala hilo, lakini badala yake huenda wakajadili juu ya hatua za kuzuia kutokea tena kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Mawaziri hao pia wanatarajiwa kujadili kurejesha mazoezi ya pamoja na mabadilishano.

Iwapo watafikia makubaliano, Japani na Korea Kusini zinatarajiwa kusonga mbele kuelekea kuimarisha ushirikiano wa kiusalama wa pande mbili, ikiwemo jibizo kwa Korea Kaskazini, inayoendelea na mipango yake ya maendeleo ya silaha za nyuklia na makombora.