Wakuu wa kijeshi wa Marekani na China kukutana wakati wa mkutano wa usalama nchini Singapore

Wizara ya Ulinzi ya Marekani inasema Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin anapanga kukutana na mwenzake wa China, Dong Jun, wakati wa mkutano mkuu wa usalama nchini Singapore.

Wizara hiyo ilisema katika taarifa yake jana Ijumaa kwamba mkutano huo umepangwa kufanyika pembezoni mwa Majadiliano ya Shangri-La, yatakayoanza Mei 31.

Utakuwa ni mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kati ya viongozi wakuu wa wizara za ulinzi wa nchi hizo mbili tangu Novemba mwaka 2022. Austin na Dong walizungumza kwa njia ya video mwezi uliopita.

Hatua hiyo ilikuja kufuatia Rais Joe Biden wa Marekani na Rais Xi Jinping wa China kukubaliana kurejesha majadiliano kati ya viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi kwenye mkutano wao mwezi Novemba mwaka jana.

Austin na Dong wanatarajiwa kujadili masuala ya Taiwan na Bahari ya China Kusini kwenye mkutano wao. China inazidi kuishinikiza Taiwan kupitia mazoezi ya kijeshi kwenye maeneo yanayoizunguka Taiwan, na inaendeleza tabia za kichokozi kwenye Bahari ya China Kusini, ikiwemo kurusha mizinga ya maji kwenye meli za Ufilipino.