Mawaziri wa fedha, magavana wa benki kuu wa G7 wajadili uchumi wa dunia

Mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu wa ya Kundi la Nchi Saba Zilizostawi Zaidi Kiviwanda Duniani G7, wamekutana kwa siku mbili za mazungumzo. Wanatahadharisha kuhusu uzalishaji kupita kiasi nchini China.

Mkutano huo ulianza jana Ijumaa kaskazini mwa Italia. Wajumbe wanajadili uchumi wa dunia.

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulionekana kuwa hatari kubwa zaidi. Baadhi ya wajumbe pia walisema wana wasiwasi juu ya uzalishaji mkubwa wa China wa magari ya umeme na bidhaa zingine.

Sarafu ya yeni ya Japani imeporomoka katika miezi ya hivi karibuni. Wawakilishi wa nchi hiyo walisisitiza utambuzi wa G7 kwamba viwango vya kubadilisha fedha vinavyobadilika kupita kiasi vinaweza kuathiri utulivu wa kifedha.

Naibu Waziri wa Fedha wa Masuala ya Kimataifa wa Japani, Kanda Masato aliwaambia wanahabari kwamba Japani ipo katika mawasiliano ya karibu na nchi zingine, hasa Marekani.

Alisema hakuna haja ya kuingilia kati ilimradi masoko yako imara, lakini serikali itachukua hatua zinazofaa ikiwa mabadiliko ya haraka yataathiri vibaya uchumi.

Leo Jumamosi itashuhudiwa wajumbe wakijadili jinsi ya kushughulikia mali za Urusi zilizoshikiliwa kama sehemu ya vikwazo kutokana na mzozo wa Ukraine.