Maswali na Majibu: Cha kufanya maji yanapokatika (5) Kuzuia kurudi kwa majitaka

NHK inajibu maswali kuhusiana na kukabiliana na majanga. Nchini Japani, maji salama ya bomba hupatikana muda wote. Lakini watu hukabiliwa na usumbufu mkubwa pale tetemeko la ardhi ama majanga mengine yanaposababisha maji kukatika. Katika mfululizo huu, tunakuletea taarifa zitakazokusaidia kuchukua hatua kwa utulivu pale maji yanapokatika. Leo hii, tunaangazia namna ya kuzuia kurudi kwa majitaka.

Wakati mafuriko yanapotokea, kurudi kwa majitaka ni suala linaloibua wasiwasi sambamba na kukatika kwa maji. Kurudi kwa majitaka hutokea wakati nyumba zinapofurika na maji katika mifereji ya majitaka kutiririka kwa kurudi nyuma. Pale maji machafu yanapotoka nje ya mabomba ya mabafu, vyooni na mashine za kufulia nguo, usafishaji wake huwa ni shida. Vijidudu na virusi vinaweza kusababisha magonjwa, na harufu mbaya yaweza kusalia.

Mifuko ya maji inasaidia kuzuia majitaka kurudi. Mfuko wa maji unaweza kutengenezwa kwa kutumia mifuko mikubwa ya taka ambayo kaya nyingi huwa nayo tayari. Ingiza mfuko mmoja wa taka ndani ya mwingine na ujaze maji hadi nusu. Ondoa hewa na ufunge mfuko huo. Ili kuzuia majitaka kurudi vyooni, funika sehemu ya juu ya choo cha kukalia kwa kutumia mfuko tupu na weka mfuko wenye maji juu yake. Hii ni mbinu inayoshauriwa na serikali kuu na serikali za maeneo.

Kuhusu muda wa kuchukua tahadhari hii, ni bora zaidi kuichukua mapema panapokuwa na mashaka ya mafuriko. Kama utasikia sauti za kububujika kwa maji kwenye choo chako ama ukihisi harufu mbaya, hiyo inaonyesha kuna hatari ya kurudi kwa majitaka hivyo unapaswa kuwa makini zaidi. Kando na vyoo, chunguza pia mabomba mengine nyumbani kwako. Weka mifuko ya maji kwenye sehemu ya kunawia, mashine ya kufulia, sinki la jikoni na mahali pengine penye uwazi. Hii itasaidia kuzuia kurudi kwa majitaka.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Mei 24, 2024.