Rais Macron wa Ufaransa asimamisha mswada wa marekebisho ya upigaji kura eneo la New Caledonia

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alizuru eneo la New Caledonia jana Alhamisi na kutumia siku hiyo akijaribu kutafuta njia ya kumaliza machafuko yaliyodumu zaidi ya juma moja. Alifanya mkutano na wanahabari katika mji mkuu wa Noumea leo Ijumaa na kusema, kwa sasa, hatalazimisha kutekelezwa kwa sheria iliyozua machafuko hayo.

Macron aliongeza kuwa ni matumaini yake kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja, machafuko hayo yatamalizika na kwamba makubaliano ya pamoja baina ya watu katika eneo hilo yatakuwa “yamesonga mbele.”

Wabunge katika bunge la Ufaransa walichochea machafuko hayo juma lililopita kwa kupitisha mswada mpya. Wanataka kupanua haki za kupiga kura ili kujumuisha watu walioishi katika eneo hilo kwa miaka isiyopungua kumi.

Hata hivyo, makundi yanayopendelea uhuru hasa watu wa Kanak ambao ni wenyeji na ni karibu asilimia 40 ya watu wote katika eneo hilo, wanapinga mpango huo. Wanahofia kuwa mabadiliko hayo huenda yakawanufaisha wapiga kura wanaopendelea Ufaransa.

Macron alipeleka maelfu ya maafisa wa usalama kukomesha machafuko hayo. Alisema watasalia “kwa muda mrefu kadiri inavyohitajika” ili kurejesha utulivu.

Aliwataka viongozi wa pande zote mbili kutoa wito wa utulivu na kuanza tena mazungumzo. Alisema yuko tayari kusubiri kwa wiki chache kwa wao kutafuta suluhisho, ingawa aliongeza kwamba mswada wa marekebisho ya upigaji kura si kitu cha “kutupilia tu mbali.”

Macron alikiri kuwa wakazi wengi wanakabiliwa na ubaguzi zaidi. Baadhi ya watu wa jamii ya Kanak wanasema watu wanazungumzia usawa, lakini wao wenyewe wanaamini “haujawahi kuwepo.”