Kiwango cha ajira kwa wahitimu wapya wa vyuo vikuu nchini Japani kipo juu zaidi tangu mwaka wa fedha 1996

Utafiti wa serikali ya Japani unaonyesha kuwa asilimia 98.1 ya watu waliohitimu vyuo vikuu mwezi Machi mwaka huu wamepata kazi. Idadi hiyo ni ya juu zaidi tangu mwaka wa fedha 1996, ulipoanza utafiti wa kila mwaka.

Wizara za kazi na elimu zilitafiti watu 6,250 waliosoma katika vyuo vikuu 112 na taasisi zingine kote nchini Japani kuhusu shughuli zao za kutafuta kazi kufikia Aprili Mosi mwaka huu.

Matokeo yalionyesha kiwango cha ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu kilikuwa asilimia 98.1, juu kwa asilimia 0.8 kutoka wakati huo huo mwaka jana.

Kwa jinsia, asilimia 97.9 ya wanaume walipata kazi, ikiwa ni asilimia 0.6 zaidi ya mwaka jana, kwa wanawake ni asilimia 98.3, ikiwa ni asilimia 1 zaidi.

Waziri wa kazi wa Japani Takemi Keizo aliwaambia wanahabari kwamba idadi inayoongezeka ya makampuni yanaajiri wafanyikazi kwa bidii huku kukiwa na uhaba wa wafanyakazi.

Takemi alisema serikali inakusudia kuwasaidia wahitimu, ambao bado wanatafuta ajira, kupitia huduma za upangaji kazi za umma na programu zingine.